Posted By Posted On

Matonya atamba kufanya muziki kama starehe

NA JEREMIA ERNEST

HUYU hapa Seif Shaban a.k.a Matonya, miongoni mwa wasanii wachache waliochochea mabadiliko chanya kwenye Bongo Fleva haMatonya atamba kufanya muziki kama starehesa nyimbo za mapenzi.

Matonya amewahi kutikisa chati za muziki kwa ngoma zake kama Vaileth, Taxi Bubu, Spea Taili, Anita na Dunia Mapito ambao ni wimbo bora wa muda wote unaotumika kila unapotokea msiba hapa Bongo.

Msanii huyo alizaliwa Hospitali  ya Bombo mkoani Tanga ambapo ndipo asili yake na alihitimu shule ya msingi Mkwakwani.

Alijiunga na sekondari ya Kahare na hakufanikiwa kumaliza kidato cha nne kwa sababu ambazo hakutaka kuziweka wazi.

Anasema alifunga ndoa na kupata mtoto mmoja wa kiume ila mwanamke huyo kwa sasa wametengana.

ALIVYOINGIA KWENYE SANAA

Ameeleza safu hii kuwa alianza muziki akiwa shule ya msingi kwa kuimba kwenye bendi ya shule.

“Nilikuwa miongoni mwa wanafunzi ambao walikuwa kwenye bendi ya shule huko ndipo nilipoanza kujikita katika tasnia hii,” anasema Matonya.

Anasema baada ya kumaliza shule ya msingi alipofika sekondari aliingia kwenye sanaa ya kuruka sarakasi hivyo akawa na vipaji viwili.

Baada ya kumaliza shule walianzisha kundi la muziki  na wenzake wa tatu walijipa jina la Hard Boy Family wakaenda kushiriki kwenye shindano la kuibua vipaji Tanga.

“Tulishiriki katika shindano la vipaji vya muziki tukashika nafasi ya pili hapo ndipo mafanikio ya muziki yalipoanzia,” anasema Matonya.

Mmoja ya zawadi waliyopata ni kurekodi hivyo walitoka Tanga hadi jijini Dar es Salaam walitoa ngoma ambayo ilifanya vizuri kidogo.

Anasema alipokuja Dar es Salaam, alijiongeza akafanya nyimbo moja  Uwaminifu, hii ndio ilimfanya akaanza kupata shoo katika kumbi za starehe.

“Baada ya kutoa ngoma hiyo nilifanikiwa kufanya albamu ya kwanza ikafata ya pili Siamini Macho Yangu 2003 ndani yake kulikuwa na wimbo wa Vaileth,” anasema.

FAIDA NA CHANGAMOTO ZA MUZIKI

Ameeleza kuwa wakati anaanza alikutana na changamoto ya kukosa msimamizi na mfadhili ilimbidi ajichange mwenyewe ili kuingia studio.

“Nilianza kufanya muziki kwa mapenzi nachukua fedha naenda studio wakati huo sina uhakika kama itarudi,”.

Aliongeza kuwa Tanga hakukuwa na studio ili mlazimu kuja Dar es Salaam ili arekodi hii ilikuwa inaumiza kwa kuwa gharama ilikuwa juu kutokana mazingira.

Kwa upande wa faida anasema muziki umempatia utajiri wa watu anafahamiana  na wakubwa, wadogo, mataji na masikini.

“Nimepata nafasi ya kujuana na watu wengi kutokana na sanaa imekuwa rahisi kufanya biashara zangu,” anasema Matonya.

Mbali na hilo amepata rasilimali nyingi kupitia muziki ambazo zimempatia heshima kuishi maisha mazuri ya kumiliki nyumba na gari.

SABABU ZA KUKAA KIMYA

Anasema biashara ya muziki imekuwa ikibadilika kila wakati tofauti na ilivyoanza anza, sasa hivi hata vyombo vya habari vinamiliki wasanii wake.

Aliongeza kuwa wale aliokuwa  anafanya nao kazi wameacha wamekuja wapya ambao nao wana wasanii wao walioingia nao mkataba.

“Kila mdau wa muziki ana msanii anaye msaidia wengine wameunda makundi inakuwa ngumu kupata  nafasi tusiokuwa na lebo,” anasema Matonya.

Ameelaza kuwa biashara anazofanya zimechangia kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ana kosa muda wa kufanya muziki  kwa ushindani.

YUPO WAPI?

Anasema kwa sasa anaishi Bahari Beach jijini Dar es Salaam japo kuwa makazi yake mengine  yapo Tanga na Nairobi, Kenya ambako huko kuna baadhi ya miradi anafanya.

Kuhusu muziki kwa sasa ametoa ngoma yake Kanikaa aliomshirikisha Christian Bella huku akitamba kuwa anafanya sanaa kama starehe sio biashara tena kama alivyokuwa anafanya mwanzoni.

“Muziki kwangu ni starehe, ninapojisikia naingia studio narekodi natoa ngoma ikawaburudishe mashabiki zangu ambao wanapenda ninachokifanya,” anasema Matonya.

Kwa sasa anafanya biashara ya kuuza magari pamoja na nyumba.

Anasema hali ya muziki nchini ipo vizuri kwa wale ambao wana wezeshwa ila kwa wengine ni ngumu kwa kukosa watu wa kuwashika mkono.

Aidha alimpongeza msanii, Hamonize kwa hatua aliyofikia na kumtaka asikate tamaa na aendelee kupambana kuyafukuzia malengo.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *