Posted By Posted On

MMEMCHOKOZA:MTAMKOMA MO DEWJI,Plani zake mbili za kumvuruga Hersi na GSM yake zavuja

NA MICHAEL MAURUS

MAMBO ni moto ndani ya Simba, ikielezwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’, amepania kufanya makubwa ili kuwakata ngebe wale wote wanaoleta chokochoko Msimbazi.

Mara baada ya Bodi ya Wakurugenzi Simba kumteua Barbara Gonzalez kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo, kuna baadhi ya wadau walikuwa wakiponda uamuzi huo wakidai umelenga kutetea maslahi binafsi ya Mo.

Akizungumzia uteuzi huo wa Barbara, Mo Dewji alisema: “Hatujakurupuka kufanya maamuzi na wala sio maamuzi yangu, ni ya kikao kwani tulikaa na kuamua kumpitisha Barbara, anakuwa CEO wa kwanza mwanamke. Ni mchapakazi na anaipenda Simba, hivyo tunaamini kila kitu kitakwenda sawa.”

Kwa upande wake, mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Asha Baraka ‘Iron Lady’, alisema hawakukurupuka hata kidogo katika uamuzi huo kwani

kabla ya Barbara kupewa ‘shavu’ hilo, alikuwa majaribioni kwa kuratibu mchakato mzima wa tamasha la Wiki ya Simba na hatimaye kilele cha tukio hilo, maarufu kama Simba Day.

Alisema kuwa kutokana na jinsi alivyofanikiwa kufanikisha tamasha lao, wao kama bodi wakaona kuna kila sababu ya kumteua Barbara kuwa C.E.O wa Simba, wakiamini ana uwezo na sifa ya kuwafikisha pale wanapokusudia ambako si kwingine, bali kuifanya klabu yao kuwa tishio Afrika.

Katika kile kinachoonekana kuwajibu wale wote waliomchokoza Mo kutokana na uteuzi wa Barbara, lakini pia kukata ngebe za watani wao wa jadi, Yanga ambao wamekuwa wakitamba kufanya makubwa msimu huu, Mo Dewji amekuja na mkakati kabambe wa kuwapa raha Wanamsimbazi.

Akizungumza na BINGWA wiki iliyopita, Barbara alisema kuwa mkakati wa kwanza wa Mo ilikuwa ni kumwezesha yeye na mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mulamu Ng’hambi kufanya ziara Misri kwenda kuvuna ‘maujuzi’ kwa vigogo wa soka Afrika, Al Ahly na Zamalek.

Ziara hiyo ililenga katika kujifunza namna ya uendeshaji wa klabu ili iwe na mafanikio, kuanzia ndani hadi nje ya uwanja, Barbara akikiri kupata nondo za nguvu ambazo zitaibeba mno klabu yao.

“Tumejifunza mengi katika ziara yetu ya Al Ahly na Zamelek, tumetembezwa katika kila idara ya klabu hizo hadi kwenye viwanja vyao kujionea jinsi wanavyoziendesha klabu zao, hakika tumepata ujuzi wa kutosha ambao tunaanza kuufanyia kazi mara moja kuifikisha Simba pale wenzetu hao walipo,” alisema Barbara.

Alisema baada ya kutoka Misri, wamepanga kufanya ziara nyingine Ulaya ili kwenda kuvuna ujuzi zaidi kwa klabu za huko, zikiwamo Liverpool, Juventus, Manchester City, Everton, Porto na nyinginezo.

Ukiachana na jeuri hiyo ya Mo Dewji ya kufanikisha ziara ya Barbara na Mulamu nchini Misri, pia mfanyabiashara huyo ana kiu ya kuona kikosi chao kitatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya nne, ikiwamo kufika nusu fainali na hata fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Mo anaonekana amepania kufanya mambo makubwa ili kuwaumbua wale ambao wamekuwa wakikosoa baadhi ya mambo ndani ya Simba. Ukiachana na ziara zilizofanywa na CEO nchini Misri, Mo ameweka wazi shauku yake ya kuona tunaifunga Yanga mabao zaidi ya matano tutakapokutana nao.

“Kila unapoongea naye, atakwambia kuwa huwa anaifikiria sana Simba, akiwaza ni vipi anaweza kuifanya kuwa tishio Afrika. Pia, japo hapendi kusema wazi wazi, Mo ana kiu ya kuifunga Yanga mabao zaidi ya matano. Nina wasi wasi, hilo linaweza kutokea tutakapocheza na Yanga. Ninaamini iwapo atakutana na wachezaji na kuwapa maneno yake, Yanga watakoma,” alisema mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba alipozungumza na BINGWA wikiendi iliyopita.

Alisema mambo hayo mawili, Simba kuendelea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo na kuipa Yanga kipigo cha nguvu, ndiyo yaliyopo akilini mwa Mo Dewji, akiamini hapo ndipo mashabiki, wanachama na viongozi wa Wanajangwani hao, akiwamo Hersi Said wa GSM, watakapokubali kuwa Wekundu wa Msimbazi ni kiboko.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *