Posted By Posted On

Mwambusi ataja kilichoiua Stars, Ndayiragije akiri

 NA WINFRIDA MTOI

KOCHA msaidizi wa timu ya Yanga, Juma Mwambusi, ametaja sababu ya timu Tanzania, Taifa Stars, kufungwa na Burundi kuwa ni kucheza kwa kufuata mfumo wa wapinzani.

Mwambusi alikuwa miongoni mwa makocha walikuwa uwanjani kufuatilia mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati Stars na Burundi uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ulioshudiwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, Taifa Stars ilikubali kipigo cha bao 1-0.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mwambusi alisema Burundi walicheza kwa kupooza mpira na mtego wao ukafanikiwa kunasa kwa Stars na kufuata mfumo wanaocheza.

Mwambusi alisema Taifa Stars ilitakiwa kucheza mpira wake kwa kuchangamka, lakini si kufuata mipango yao ambayo imesababisha kupoteza mchezo.

“Mpira ulikuwa mzuri kiasi, ila kipindi cha kwanza Burundi walitulazimisha kucheza kama wanavyotaka wao na sisi tukaingia mtegoni kwa kucheza mpira uliopoa, watuangalie tunafanya nini, watushambulie kwa kushtukiza,”alisema Mwambusi.

Alisema kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Taifa Stars kipindi cha pili yalichangamsha mchezo na kutengeneza nafasi,  lakini kulikuwa hakuna utulivu na kadi nyekundu ya Jonas Mkude ilichangia.

 “Kitu kingine katika safu ya ushambuliaji kulikuwa hakuna uwiano mzuri, nadhani kiungo ilishindwa kuwalisha vizuri washambuliaji, mwalimu ameliona hilo atakwenda kulifanyia kazi,” alisema Mwambusi.

Akizungumzia mchezo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, alisema timu inaanza kwenda kule anakotaka, lakini bado suala la umakini limekuwa shida kwa nyota wake.

Alisema matokeo ya kufunga yamempa changamoto ambayo alikuwa anahitaji kuona kuelekea katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Tunisia.

“Tunahitaji kufanya kazi zaidi katika eneo la kiungo na umaliziaji, hii ni changamoto na tunahitaji zaidi kutengeneza nafasi na kuzitumia,”alisema Ndayiragije.

Ndayiragije alisema atazungumza na uongozi kupata muda mwingi wa kukaa na wachezaji ili aweze kufanya kile anachohitaji.

Kwa upande wake,  Kocha Mkuu wa timu ya Burundi, Ndayizeye Jimmy, alisema Taifa Stars ilikuwa juu zaidi yao na walipata shida kutafuta bao hilo kwa sababu wamekutana na kikosi kinachowafunga mara nyingi.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *