Posted By Posted On

OFFICIAL NGOMA:Kipaji kipya Bongo Fleva aliyetendewa haki na Mr Blue

NA GLORY MLAY

MWISHONI mwa mwaka 2014 katika Ukumbi wa Club Billcanas, jijini Dar es Salaam, kuna tukio lililomtokea kijana mmoja ambalo lilikuwa la kufurahisha.

Ilikuwa siku ya Sikukuu ya Krisimas ambayo kulikuwa na disco la watoto lililoanza saa sita mchana mpaka saa 12 jioni, likitumbuizwa na wasanii mbalimbali wa Bongo Fleva.

Kijana mmoja aliyekuwapo kwenye ukumbi huo, alipomuona msanii wa Bongo Fleva, Khery Sameer ‘Mr Blue’, alitoka mbio na kumfuata ili aweze kumsalimu.

Mbio za kijana huyo zilizaa matunda baada ya kufanikiwa kumsimamisha nyota huyo ambaye alikuwa amepanda kwenye gari lake tayari kuondoka eneo hilo.

Kijana huyo anasema alifanikiwa kumsalimia na kujitambulisha kwake na kuomba sapoti kwani ndio alikuwa anaanza sanaa ya muziki.

“Nilipokuwa kule ndani Billcanas, nikamwona Mr Blue anatoka, ndipo nikamkimbilia ili nimsalimu kwani ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kumuoa, nilikuwa namsikia tu kwenye redio na kumuona kwenye TV.

“Nilipomkaribia, nilimwita, aligeuka na kuniangalia na kuitikia salamu yangu, akanipa mkono na kuniuliza shida yangu ilikuwa nini? Nikamwambia kuwa ninahitaji sapoti yake na ushauri kwenye kazi yangu,” anasema.

Kijana huyo si mwigine, bali ni Abbas Miasara ‘Official Ngoma’ mbaye amejikita katika muziki baada ya kugundua kipaji chake tangu akiwa shule.

Official Ngoma, ametoa simulizi hii jana alipotembelea ofisi za New Habari (2006) Limited, wazalishaji wa magazeti ya BINGWA, DIMBA, MTANZANIA, RAI na Mtanzania Digital.

Katika mahojiano hayo, Official Ngoma alielezea mengi kuhusiana na muziki, lakini pia historia yake.

Juu ya historia yake, msanii huyo anasema kuwa alizaliwa mkoani Iringa na kufanikiwa kuhitimu masomo yake ya darasa la saba mwaka 2008, katika Shule ya Msingi Ubungo Msewe, Dar es Salaam.

Baadaye alijiunga na kidato cha kwanza ST. Magreth Mbagala, jijini Dara es Salaam na kuhitimu mwaka 2012.

Baada ya kuhitimu kidato cha nne, Official Ngoma anasema alijiunga na taasisi ya kuibua vipaji vya muziki hapa nchini ya Tanzania House of Talent (THT).

“Nilivyomaliza kidato cha nne, mambo hayakuwa mazuri, nikaamua kujiunga na THT kwa lengo la kujiboresha zaidi katika muziki ambao nilipanga kuufanya. Nilijifunza mengi kwasababu nilikutana na wasanii wa kila aina,” anasema.

Anasema baada ya kupata ujuzi wa kuandika mashairi na kuimba, alifanikiwa kupata uongozi ambao ulikubali kumsimamia yeye pamoja na kazi zake.

Ngoma anasema alitangazwa rasmi katika uongozi huo wa Ngoma Empire ambao unaongozwa na mmoja wa msanii wa filamu hapa nchini, Daudi Michel’ Duma’, akiwa ndiye msanii wa kwanza Japo wengine wapo lakini bado hawajatangazwa.

“Baada ya kumalizana na THT, namshukuru Mungu nilipata uongozi ambao uliniahidi kufanya kazi na mimi na tuliingia makubaliano na sasa nipo chini yao. Nilisikia fahari kubwa kuona sijapitia changamoto nyingi kama walivyo wenzangu,” anasema.

Anasema akiwa na uongozi huo, amefanikiwa kutoa wimbo katika mfumo wa audio na video unaokwenda kwa jina la ‘Sawa’, iliyofanywa na Lizer wa  Wasafi Records, huku video ikiwa chini ya Hanscana.

Ngoma anasema wimbo huo una wiki moja tangu autoe na umepokewa kwaida, akiwataka mashabiki kuendelea kumsapoti ili kufika mbali.

“Nina wimbo wangu ambao upo katika mitandao ya kijamii, una wiki moja tangu utoke, lakini mapokezi si makubwa sana, lakini ninaamini mashabiki na wadau wa muziki watanisapoti ili kufika mbali zaidi,” anasema.

Anasema amekuwa akipata sapoti kubwa kutoka kwa Mr Blue kwani amekuwa akimshauri mambo mbalimbali katika kazi yake hiyo.

“Tangu nimfahamu, amekuwa akija studio mara kwa mara kuona ninachofanya, amekuwa akisikiliza nyimbo zangu na kunishauri vitu vingi vya kuongeza au kupunguza, amekuwa akinitafutia dili mbalimbali, namshukuru sana kwa kuacha kazi zake na kunisapoti,” anasema.

Ngoma anasema kuwa ili kufika mbali katika kazi yake, anatamani kufanya kolabo na Naseeb Abdul ‘Diamond Platinumz’.

Anasema amemchagua huyo kwasababu ni msanii ambaye anafahamika kimataifa hivyo atamfanya na yeye kujulikana na pia kupata mashabiki wengi kutokana na umaarufu wake.

Anasema pia Diamond amekuwa akijitolea kusapoti vijana na wengi wamefanikiwa kufika mbali katika kazi hiyo ya muziki.

“Ninaamini nikifanya kazi na Diamond, nitajulikana mara moja kitaifa na kimatiafa, pia kazi zangu zitakuwa zikifuatiliwa kila siku na mashabiki wataongezeka,” anasema.

Mbali ya yote hayo, Ngoma anasema kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo anakutana nazo kwenye kazi yake hiyo ya muziki.

Anasema kuwa moja ya changamoto hizo ni ushindani kuwa mkubwa hivyo kushindwa kupata nafasi ya kuonekana.

“Unakuta leo nimetoa wimbo na Diamond katoa wa kwake, unajua fika kuwa watu lazima wasikilize ya Diamond, ni wachache sana ambao watanisapoti, vitu kama hivi vinatuumiza ila tunajua siku moja tufika,” anasema.

Anasema kuwa changamoto nyingine inawafanya chipukizi kutumia nguvu nyingi kujitangaza tofauti na miaka ya nyuma kwasababu wasanii wamekuwa wengi.

Ngoma anasema matarajio yake ni kufika anga ya kimataifa zaidi kama walivyo wasanii wakubwa hapa nchini.

Anasema anajiamini na anaamini kile anachokifanya na anajua kuwa ipo siku atafikia malengo hayo, hivyo anaendelea kupambana na kuweka juhudi binafsi katika kazi zake.

“Kila mtu ana ndoto za kufika mbali, lakini wengi hawafiki kwani wanakata tamaa mapema, nitapambana kuhakikisha kazi zangu zinafika kimataifa zaidi,” anasema.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *