Posted By Posted On

Ujumbe wa Kaze Yanga huu hapa

ASHA KIGUNDULA NA WINFRIDA MTOI

KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, Cedric Kaze raia wa Burundi, anatarajia kuwasili nchini kesho au keshokutwa usiku tayari kuanza majukumu yake, huku akiwa ametuma ujumbe ‘bab kubwa’ kwa wachezaji wa timu hiyo pamoja na viongozi.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa kocha huyo ataunganisha safari yake hadi Mwanza kukifuata kikosi chake ambacho kitaweka kambi jijini humo kuiwinda Polisi Tanzania watakayokutana nayo Oktoba 22, mwaka huu.

Mchezo huo dhidi ya Polisi Tanzania utakuwa ni wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ukipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Mtoa habari wetu wa uhakika, amelipasha BINGWA kuwa Kaze atawasili nchini  akitokea Canada na moja kwa moja kusaini mkataba na Yanga tayari kuanza kazi.

“Kocha anawasili Jumatano au Alhamis, kila kitu kipo sawa, akiwasili moja kwa moja atakutana na viongozi wetu na kusaini mkataba wa kuanza kazi ya kufundisha timu yetu hii pendwa ya Yanga,” alisema.

Hata hivyo, mtoa habari wetu alisema katika makubaliano yao na kocha huyo kwanza watampa mkataba wa muda mfupi na baadaye watamwongeza, ikiwa baada ya kuona mabadiliko ya timu yao.

Japo hajatua nchini, lakini tayari Kaze ameanza kazi Yanga tangu akiwa Canada, akiwa ameongea moja kwa moja na wachezaji pamoja na viongozi wa benchi la ufundi kupitia video.

Mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi, ameliambia BINGWA kuwa Kaze ametoa maelekezo yake ambayo yanatakiwa kufuatwa na wachezaji pamoja na viongozi ili kurahisisha kazi yake.

Moja ya ujumbe aliotuma kocha huyo, ni wachezaji kuzingatia nidhamu kuanzia ndani hadi nje ya uwanja, kujituma kadri ya uwezo wao, kuithamini jezi ya Yanga pamoja na mashabiki wa klabu hiyo.

“Huyu kocha anaonekana ana msimamo sana, maana amesema mchezaji ambaye atakwenda kinyume na maagizo yake, hatapata nafasi katika kikosi chake hata awe na uwezo kiasi gani.

“Pia, amewataka wachezaji wazawa wajitafakari kwa kila mmoja kupigania namba kikosi cha kwanza kwani hawezi kukubali kuona wageni ndio wanatawala katika kikosi chake akifahamu Tanzania kuna vipaji vingi tu,” alisema.

Imeelezwa kuwa kocha huyo pia hajawaacha viongozi wa Yanga, akiwataka kutomwingilia katika kazi yake, ikiwamo kupangiwa kikosi.

Baada ya Yanga kukipiga na Polisi Tanzania Uwanja wa Mkapa, kikosi hicho kitakwea pipa kwenda Mwanza kuikabili KMC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, kisha Biashara United, Dimba la Karume, Mara.

Katika michezo yote hiyo, Kaze anatarajiwa kuwa kwenye benchi, lakini ambayo atakuwa na muda mwingi kukiandaa kikosi chake ni dhidi ya Simba itakayochezwa Novemba 7, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambaye ni wadhamini wa Yanga, Mhandisi Hersi Said, alithibitisha kuwa kocha wao huyo atawasili Alhamisi.

Alisema kila kitu wamemaliza, hivyo Wanayanga wajiandae kumpokea  na kumpa ushirikiano katika kukijenga kikosi chao.

“Kocha nakuja Alhamisi kama hakutakuwa na changamoto yoyote, kila kitu tumekamilisha, iliyobaki ni kumpokea. Wapenzi wa Yanga watarajie kumuona mechi ijayo, kama atakamilisha vibali mapema atakuwa mwenye benchi,” alisema.

Alieleza kuwa wamemchagua kocha huyo kuinoa Yanga kutokana na vitu vingi alivyonavyo, akiamini ataisaidia klabu katika mambo mengi.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *