Posted By Posted On

HIZI HAPA REKODI ZA KUTISHA, MSHAMBULIAJI MPYA YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Yanga juzi ilikamilisha usajili wa Said Ntibazonkiza, raia wa Burundi kwa mkataba wa miaka miwili ikiwa ni saa chache tangu alipoifunga timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Jumapili, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Burundi kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Baada ya kusaini mkataba mshambuliaji huyo alisema: “Ninayo furaha ya kusaini mkataba katika timu kubwa ya Yanga, nadhani kutokana na uzoefu nilionao na kushirikiana na wachezaji wenzangu inshallah tutaifikisha sehemu kubwa pale uongozi na wapenzi wanapohitaji. Daima mbele, nyuma mwiko.”

Naye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni ya GSM inayoidhamini Yanga, Hersi Said alisema walianza kumfuatilia mchezaji huyo kwa muda mrefu, lakini hawakufanikiwa kuinasa saini yake.

“Alikuwa na mkataba na klabu yake (Vital’O ya Burundi), tulijaribu kuzungumza nao lakini ikashindikana kumuachia na muda haukuwa rafiki kwetu, lakini hivi sasa yupo huru,” alisema Hersi

Hata hivyo, Ntibazonkiza ataanza kuitumikia Yanga baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Desemba 15, kwa sababu hivi sasa haruhusiwi kucheza kutokana na muda wa usajili wa dirisha kubwa kupita.

Ntibazonkiza (33), amezichezea timu za Vital’ O FC alikodumu tangu 2003 hadi 2005, kisha alitimkia NEC Nijmegen tangu 2006 hadi 2010 na baadaye kujiunga KS Cracovia.

Akiwa NEC Nijmegen ya Uholanzi, mchezo wake wa kwanza alicheza ilipopambana na FC Dinamo kwenye Kombe la UEFA na kufanikiwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Baada ya kuonyesha kiwango kizuri, kocha wa NEC Nijmegen, Mario Been alimtoa kwenye kikosi cha vijana alikopelekwa kwa ajili ya mazoezi na kujiunga na timu ya wakubwa.

Ntibazonkiza aliyewahi kutesa na klabu za nchini Ufaransa, Uturuki na Uholanzi – timu nyingine alizowahi kuzichezea ni Kaysar Kyzylorda, Akhisar Belediye, SM Caen, Kysar na anatua Yanga akitokeoa Vital’O.

Mchambuzi wa soka, Ali Mayayi akizungumzia usajili huo alisema usajili huo anauona kuwa unatokana na kila kocha kuwa na jicho lake kwa wachezaji kulingana na timu anayofundisha.

“Usajili uliofanywa (dirisha kubwa) labda haujakidhi mahitaji ya timu, ndio maana wameona waongeze mtu wa kuwasaidia hasa eneo la ushambuliaji,” alisema Mayay.

“Siku zote usajili unaofanywa mashabiki wanafananisha mchezaji anayekuja na anayeondoka na inaonekana nafasi ya Amisi Tambwe na Hertier Makambo hazijazibwa.”

Mayay alisema usajili huu inawezekana ikawa ni ingizo la kocha anayetarajiwa kutua Yanga, Cedric Kaze na uongozi baada ya kuwafuatilia wachezaji mechi tano walizocheza Ligi Kuu na kugundua kuna upungufu

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *