Posted By Posted On

MWAMNYETO AFURAHIA MAISHA NDANI YA YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Moja ya usajili uliofukuta msimu uliopita ni ule wa aliyekuwa beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto.

Mwamnyeto alivuma sana kipindio hicho chote kutokana na alikuwa akigombewa na klabu zote kubwa nchini Simba, Yanga na hata Azam FC, na hizo timu mbili kongwe nchini ndo zilipigana hasa vikumbo kuiwania saini yake.

Hata hivyo, mwishowe Yanga kupitia mdhamini GSM, ndio iliofanikiwa kuinasa saini ya beki huyo ‘kitasa’ wa timu ya Taifa, Taifa Stars kwa mkataba wa miaka miwili.

Kutokana na ubora wake, Mwamnyeto ametua tu na kufanikiwa kuingia haraka kikosi cha kwanza na akionyesha kuingia na mguu mzuri ameshapata mafanikio mbalimbali ndani ya timu hiyo.

USAJILI WAKE

Mwamnyeto anasimulia namna alivyoitosa Simba na kutua Yanga. Anasema Simjba ndio ilikuwa ya kwanza kumfuata kufanya naye mazunguko, lakini mwishowe waliishia kumwona akivaa uzi wa njano na kijani.

Anakiri siku ya usajili ilikuwa ngumu kwake na wa wakati akizungumza na viongozi wa Yanga ili kumalizana naye, Simba walipiga simu mara kwa mara, lakini akaamua azikaushie ili zisimchanganye.

“Nilikuwa nafanya mazungumzo na timu zote mbili, viongozi wa Yanga walikuwa wanazungumza na meneja wangu Kassa Mussa mara kwa mara, wakati mwingine walikuwa wananipigia simu mimi mwenyewe,” anasema Mwamnyeto nakuongeza,

“Katika mazungumzo ya hapa na pale na Yanga, wakatimiza vigezo vyote, wakati nimefika Dar es Salaam, tayari kwa kusaini mkataba nadhani viongozi wa Simba, walilishtukia hilo, wakaanza kupiga sana simu, meneja wangu akaniambia nisipokee kwa sababu zingenichanganya,” anasema.

Anasema baada ya kumalizana na Yanga na usajili wake kutangazwa na vyombo vya habari, ndipo viongozi wa Simba waliacha kumpigia simu na kumfuatilia.

USAJILI KUCHUKUA MUDA MREFU

Tetesi za Mwamnyeto za kutakiwa na vigogo hao, Simba na Yanga, zilidumu kwa muda mrefu, huku zikiwaacha wadau wa soka wakitabiri atatua wapi kati ya timu hizo.

“Dili zima lilisimamiwa na meneja wangu Kassa Mussa, mimi nilikuwa napewa taarifa kuna hiki na kile, wakati huo yeye alikuwa anawasiliana nao akiwa nje ya nchi, hivyo nisingeweza kufanya kitu chochote bila yeye,” anasema kuongeza,

“Ilikuwa inanipa wakati mgumu na mtaani nikipita, wanaanza kuniuliza naenda wapi kati ya Simba au Yanga, wengine wakiniambia dogo kuwa na msimamo wa maamuzi, maana walikuwa wanaona usajili unaongelewa sana, lakini hawaoni kama nimeamua kwenda wapi,” anasema Mwamnyeto.

Anasema baada ya meneja wake kuja nchini, mambo yakaenda fasta kwa kumalizana na Yanga, hivyo kazi ikawa imebakia kwake kuonyesha matarajio ya mashabiki uwanjani.

KUANZA KIKOSI CHA KWANZA

Anasema kabla hajasaini na timu hiyo, alianza kujikoki mapema, kujua timu inahitaji nini kutoka kwake, pia kumudu presha ya mashabiki, kwani Coastal Union alikotokea hawakuwa na wafuasi wengi.

“Nilikuwa nafuatilia mechi zao, hasa kuangalia wachezaji wanaocheza nafasi yangu kujua ubora na udhaifu wao, baada ya hapo nilikuwa nayafanyia kazi katika mazoezi yangu binafsi,” anasema.

YANGA IMEMBADILISHA VIPI

Anasema maisha ya mchezaji wa kulipwa ameyajulia ndani ya timu hiyo, kama kuzingatia ratiba ya mazoezi, chakula na kulala, ili kuufanya mwili wake kuwa mwepesi kwa ajili ya kazi.

“Tofauti na Coastal Union, niliyotokea nilikuwa na maisha ya uhuru, naamua kutembea mtaani, kushinda vijiweni, wakati mwingine sikuzingatia sana nyakati za kula au kulala tofauti na hapa,” anasema Mwamnyeto.

“Yanga tunakaa kambini, ambako kuna makomandoo, hilo linaonyesha ni kiasi gani viongozi hawataki masihara, pia inatusaidia kutujenga ili kuweza kucheza zaidi ya hapa nilipo kwani bado nina safari ndefu ya kuishi ndoto zangu za soka,” anasema.

Anasema marafiki wameongezeka, wakati mwingine inamshangaza kuona anapigiwa simu na watu, wakimwambia wanafurahia kazi yake ya uwanjani, ingawa anasema hata Coastal Union alikuwa anaambiwa hivyo, lakini si kwa ukubwa huo wa sasa akiwa Yanga.

“Kifupi nimeanza kuonja matunda yakucheza Yanga, hilo linanipa moyo wa kujituma kwa bidii nikijua kiwango changu kinafuatiliwa na mamilioni ya mashabiki, ingawa nipo makini kuwajua wale ambao wanakuja kwa manufaa na wale ambao ni wa kweli,” anasema Mwamnyeto.

MECHI YA WATANI

Itakuwa mechi ya kwanza ya watani wa jadi kwa Mwamnyeto kucheza, anakiri ina presha, lakini kinachokuwa kinamsaidia akifika uwanjani, anavaa ujasiri wa ajabu kupambana na kila timu.

“Wakati nipo Coastal Union, nimecheza na Yanga na Simba, zikiwa na mashabiki wa kutosha, kuna hofu fulani nilikuwa naipata kabla ya mechi, ila nilikuwa nikikanyaga uwanjani tu, uoga wote ulikuwa unaisha, badala yake roho yakupambana ndio ilikuwa inanitawala,” anasema Mwamnyeto na kuongeza:

“Haitakuwa mechi rahisi, kwani Simba ina wachezaji wazuri na sisi tupo vizuri, hivyo naamini atakayekuwa makini na dakika 90 ndiye atakayetoka kifua mbele na kuwapa furaha mashabiki, na nina uhakika wa asilimia 100 Yanga tutashinda,” anasema.

MALENGO YAKE YANGA

Mwamnyeto anatamani mguu wake Yanga uwe wa baraka kwa kuchukua mataji ya Ligi Kuu Bara, baada ya Simba kuchukua mara tatu mfululizo.

“Sio kwamba tu natamani tuchukue mataji ya ligi, tuna kikosi kizuri ambacho kina wachezaji wapambanaji wa kutimiza ndoto hiyo ambayo hata mashabiki wana hamu ya kuiona inatimia kwa msimu huu,” anasema.

KUCHEZA NA MAPROO

Anasema hii imemfanya kutanua uwelewa wake wa namna ya kuishi na kuwaza makubwa,

“Uwepo wao hapoa unanifanya niamini hata mimi ipo siku nitacheza nje ya nchi.”

“Pia tunapata muda wa kuwafundisha Kiswahili, kitu ambacho ni kizuri kuitangaza lugha yetu katika mataifa mbalimbali,” anasema.

PESA YAKE KUBWA

Anasema wakati wameipandisha Coastal Union mwaka 2018, alipewa pesa ya usajili Sh6 milioni na aliitumia kwa kununua kiwanja pamoja na pikipiki aliyowapa wazazi wake na nyingine akaitumia kwa matumizi yake binafsi.

“Kwa mara ya kwanza tangu nianze kucheza soka nikapata hiyo milioni 6, siku ambayo nilizishika mkononi sikuamini macho yangu, lakini nashukuru Mungu nilikuwa mtulivu kwenye matumizi, maana nimefanya vitu vya maana ambavyo vimeacha alama,” anasema.

ANAIOGOPA DAR

Anasema kama kuna kitu yupo makini nacho ni kutojichanganya na starehe za jiji la Dar es Salaam, anazoamini zinaweza kumwondoa kwenye mstari wa malengo yake ya kufika mbali, hivyo anachokifanya kama timu haipo kambini nikushinda nyumbani.

“Kama timu inakuwa haipo kambini, nikitoka mazoezini huwa nashinda ndani, kwani nakumbuka wakati nakuja huku Kocha Juma Mgunda na baba yangu, walinikanya kujua kuhangaika na mambo mengi ya Dar es Salaam ni ujinga,” anasema.

“Pia naangalia ni marafiki wa aina gani ambao wanaweza wakanijenga kwa ajili ya kufikia kile ninachokitarajia, ndio maana sitaki kabisa kuhangaika na jiji hilo, mara kwenda disko au vijiweni hautaniona na Mungu anisaidie, kwani nilisisitizwa sana na baba pamoja na kocha Mgunda,” anasema.

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *