Posted By Posted On

Huyu Barbara achana naye

NA MICHAEL MAURUS
OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, ni moto wa kuotea mbali katika suala zima la uwajibikaji, BINGWA linakupasha.

Akiwa amechaguliwa kushika nafasi hiyo baada ya kujiuzulu kwa Senzo Mbatha ambaye baadaye alitimkia Yanga, Barbara tayari ameshafanya mambo makubwa Msimbazi.

Ukiachana na mifumo ya uendeshaji soka ambayo ameshaanza kuisuka ndani ya Simba, Barbara alifunga safari hadi nchini Misri kwenda kuchota ‘maujuzi’ kwa klabu kongwe Afrika za Al Ahly na Zamalek za huko.

Katika ziara yake hiyo aliyoongozana na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Ng’hambi, Barbara alijifunza mengi ambayo ameahidi kuyafanyia kazi ndani ya klabu yake hiyo inayopatikana Mtaa wa Msimazi, Dar es Salaam.

Lakini ukiachana na hilo, Barbara amejitambulisha kama mwanamama asiyetaka masikhara katika suala zima la uwajibikaji kutokana na kuwa mfano wa kuigwa na wafanyakazi wake na wengineo.

Tofauti na ilivyo kwa watendaji wengi wa aina yake, Barbara huwa anaripoti ofisini kwake kati ya saa 12 hadi saa moja asubuhi.

BINGWA lilibaini hilo mapema wiki hii lilipowasiliana na bosi huyo wa Simba saa 12:30 asubuhi na kusema kuwa tayari alikuwa amesharipoti ofisini kwake muda huo.

“Ninapoongea na wewe tayari nipo ofisini, huwa ninawahi sana na hii ni kawaida yangu. Napenda sana kuwahi kufika ofisni ili nipate muda wa kupanga na kutekeleza majukumu yangu ya siku husika,” alisema.

Alipoulizwa na BINGWA iwapo hadi muda huo kuna mfanyakazi wake yeyote ambaye alikuwa ameshafika ofisini hapo, Barbara alijibu: “Hakuna, mimi ndio wa kwanza kufika. Mara nyingi nikiwa Tanzania huwa ninakuwa wa kwanza kufika ofisini kabla ya mtu yeyote.”

Uteuzi wa Barbara kushika nafasi hiyo Simba, ulikosolewa na baadhi ya watu ambao hawakuwa wakifahamu historia yake katika soka na kazi alizofanya ndani ya klabu hiyo.

Akizungumza na BINGWA mara baada ya kushika nafasi hiyo, Barbara alisema amekuwa karibu na soka kwa muda mrefu, akiwa na urafiki na klabu kubwa Ulaya kama Liverpool, Everton, Juventus, Porto na nyinginezo.

Pia, alisema kuwa alishiriki kwa kiasi kikubwa mchakato wa mabadiliko ya kiuendeshaji ndani ya Simba, ikiwamo kuratibu kwa mafanikio makubwa tamasha la klabu hiyo la mwaka huu, maarufu kama Simba Day.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *