Posted By Posted On

Kaze kombora Simba arusha

NA ZAINAB IDDY
MASHABIKI, wanachama na viongozi wa Simba mpo? Kuna salamu zenu kutoka kwa Kocha Mkuu ajaye wa Yanga, Cedric Kaze, kuhusiana na mambo mawili.

Kaze aliyetarajiwa kutua nchini usiku wa kuamkia leo au kabla siku hii haijaisha, ametuma salamu njema kwa wapenzi wa Yanga ambazo zinaweza kuwa mwiba mchungu kwa Wekundu wa Msimbazi.

Kocha huyo raia wa Burundi aliyetangazwa na Yanga kuchukua mikoba ya Zlatico Krmpotic, anatarajiwa kuanza kuinoa timu hiyo haraka iwezekanavyo mara baada ya kusaini mkataba.

Habari kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa Kaze atapewa mkataba wa muda mfupi kabla ya kuongezewa mwingine mnono kutegemea na mafanikio yake katika kikosi hicho chenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

Akiwa anasubiriwa kwa hamu na wapenzi wa Yanga, Kaze amezungumza na gazeti la BINGWA na kufunguka mengi, ikiwamo ubora wa wachezaji wa timu hiyo na kile alichopanga kuwafanyia Wanajangwani hao.

Juu ya wachezaji wa Yanga, kocha huyo amesema amewafuatilia kwa ukaribu kupitia mechi za timu hiyo za hivi karibuni na kubaini wengi ni wazuri wenye uwezo wa kufanikisha mipango yake nda ni ya klabu hiyo.

“Tangu usajili ulipoanza, nimekuwa nikifuatilia kwa karibuni, ninafahamu wamewasajili wachezaji kutoka Kongo (DR Congo) kama Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda pamoja na Mghana Michael Sarpong na Muangola Carlinhos (Carlos).

“Mukoko na Kisinda nilikuwa nawafahamu muda mrefu na hata Michael, huyu Muangola sikuwa nimemfahamu kabla, lakini baada ya kusajiliwa na Yanga, ndipo nikamfahamu vizuri.

Ni mchezaji mzuri ambaye naamini atakuwa mzuri zaidi kutokana na program nilizopanga ambazo tayari zimeshaanza kutekelezwa na wenzangu (msaidizi wake, Juma Mwambusi),” alisema.

Aliongeza: “Wachezaji wa Tanzania (wazawa), nao ni wazuri, naamini kwa pamoja na wenzangu wa benchi la ufundi, tutawaunganisha ili kujenga timu ya ushindi.”

Kaze hakuishia hapo, bali alitoa kauli ambayo huenda ikawa ni chungu kwa watu wa Simba aliposema kuwa msimu huu ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara utatua Jangwani tofauti na Wekundu wa Msimbazi hao wanaotamba kubeba ‘mwali’ kwa msimu wa nne mfululizo.

“Ninajivunia sana kuwa kocha ajaye wa timu hii ya kihistoria (Yanga), yenye mashabiki wa kushangaza na timu bora barani Afrika. Kwa pamoja tutafanya makubwa,” alisema Kaze.

Alisema kuwa lengo lake la kwanza ni kuipa Yanga ubingwa ili kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, akiapa kuifikisha mbali timu hiyo.

Tambo hizo za Kaze ni kama ni kombora kwa Simba ambao wamekuwa wakitembea vifua mbele wakidai hakuna cha kuwazuia kubeba ubingwa wa Bara kwa msimu wa nne mfululizo, ikiwamo kutinga nusu fainali na hata fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Yanga ilimtimua Krmpotic aliyeinoa timu hiyo kwa siku chache, ikidaiwa Wanajangwani hao kutoridhishwa na ufundishaji wake ndipo walipotua kwa Kaze.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *