Posted By Posted On

Simba yawafungia kazi watatu Yanga

NA ZAINAB IDDY
PAMOJA na kudai kutotishwa na mchezaji yeyote wa Yanga, imefahamika kuwa Simba wamebaini ilipo jeuri ya watani wao hao wa jadi, kuelekea pambano la kukata na shoka baina ya wakongwe hao wa soka nchini.

Pambano hilo la Ligi Kuu Tanzania Bara linalosubiriwa kwa hamu, linatarajiwa kuchezwa Novemba 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Japo bado kuna mechi kadhaa za ligi hiyo kwa timu hizo, lakini tayari homa ya pambano hilo imeanza ndani ya klabu zote hizo mbili.

Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa Wekundu wa Msimbazi hao, japo hawana hofu na kikosi cha Yanga, lakini kuna watu watatu ambao wameamua kuwafungia kazi ili waweze kuwaliza watani wao hao wa jadi.

Watu hao si wengine bali ni wale wanaowapa jeuri Yanga, wote wakiwa ni wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu ambao ni Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda na Carlos Carlinhos.

Kwanini wachezaji hao na si wengine? Sababu ni mbili tu; kwanza ni uwezo wao uwanjani waliouonyesha hadi sasa katika kikosi cha Yanga tangu walipotua Jangwani na nyingine ni kuwakera mashabiki na wapenzi wa Yanga kwa ujumla.

Nini Simba wamekipanga kwa wachezaji hao? Habari kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, zinasema kuwa kuna wachezaji ‘wameinunua kesi’ ya baadhi ya nyota wa Yanga.

Mtoa habari wetu ameliambia BINGWA akisema: “Pamoja na maandalizi mengine tunayoendelea nayo, kuna mikakati maalum miongoni mwa wachezaji walioomba kuachiwa baadhi ya wachezaji wa Yanga wakitamba watawadhibiti hadi waonekane si lolote.

“Yanga wanachonga sana wakiwatambia Carlinhos, Mukoko na Tuisila sasa kuna wachezaji wetu wamesema wanajipanga kuwadhibiti ili wasijekuleta madhara tutakapocheza nao.

“Kuna mchezaji mmoja ameahidi kumwonyesha kazi Carlinhos hadi aombe kutolewa. Amesema kama akipangwa siku hiyo, Carlinhos hatagusa mpira, ataambulia kukimbilia kupiga kona tu na hata hatamaliza dakika 10 uwanjani kwa shughuli atakayompa,” alisema mtoa habari wetu huyo kutoka ndani ya benchi la ufundi la Simba.

Aliongeza: “Wachezaji wetu wanaamini iwapo watawadhibiti Mukoko na Tuisila, Yanga nzima itakuwa imekufa maana hata huyo Lamine (Moro) na Bakari Mwamnyeto, wanaowategemea, watachoka kuokoa mipira kila dakika na hivyo kujifunga wenyewe.”

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wachezaji, uongozi wa Simba nao upo katika mikakati kabambe kuhakikisha wanaendelea kutamba Ligi Kuu Bara msimu huu pamoja na kufika mbali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, aliliambia BINGWA jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa kwa mikakati yao wanayoendelea nayo, hakuna wa kuwazuia msimu huu.

“Tumejidhatiti kila idara kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa. Lengo letu ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania na kutwaa kombe la Afrika.

“Tunaamini tuna wachezaji wenye uwezo wa kutupa mafanikio hayo na hata benchi la ufundi ni bora, hivyo hakuna cha kutuzuia,” alisema Barbara.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *