Posted By Posted On

KAENI MBALI NA KAZE

NA ZAINAB IDDY

BAADA ya kocha mpya wa timu ya Yanga, Cedric Kaze, kutua

nchini, bosi wa klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla, amepiga mkwara mzito kwa viongozi wenzake kuingia majukumu ya benchi la ufundi.

Kauli ya Dk. Msolla imekuja baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa, kocha aliyetimuliwa hivi karibuni na uongozi wa klabu hiyo, Mserbia Zlatko Krmpotick,  alikuwa na wakati mgumu wa kupata kikosi chake.

Ilieleza kuwa pamoja na Krmpotick kuiwezesha Yanga kushinda michezo mitano na sare moja katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hakuwa na uhuru wa kupata kikosi chake, jambo ambalo limemuibuka mapema, Dk Msolla na kukemea kwa nguvu zote  tabia hiyo ili isitokee kwa kocha mpya.

Habari zilizopatikana jana ndani ya klabu hiyo, zilieleza kuwa, pamoja na viongozi wa Yanga kutoridhishwa na utendaji wa Mserbia huyo, lakini alishindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo kutokana na kupangiwa kikosi.   

Chanzo kiieleza kuwa ilifika wakati kocha huyo Msebia, aliyetimuliwa alikuwa anashindwa kuelewa nini afanye na achukue lipi kutokana na kila kiongozi wa klabu hiyo kutaka apange kikosi anachohitaji kicheze.

Hata hivyo, Dk Msolla alisema hatarajii kuona wala kusikia kocha wao mkuu mpya akiingiliwa katika majukumu yake yakiwamo ya kupangiwa kikosi na mtu yeyote.

Dk.  Msolla alisema moja ya mambo asiyotamani kuyaona yanatokea katika klabu hiyo ni Kaze kuingiliwa majukumu yake, kwani kutamfanya kazi pasipo uhuru..

“Naujua mpira wa Tanzania, viongozi tunaouongoza na mashabiki wake,  binafsi sitaki kuona wala kusikia taarifa ya kocha kuulizwa kwanini mchezaji fulani hajacheza, hampi nafasi au amemuanzisha.

“Nasema haya kwa sababu kocha tuliyemuamini kumpa timu ndiye anayejua yupi wa kumtumia katika mchezo yupi na sababu gani, yupo  fiti au hayupo fiti, lakini kwa sababu kuna baadhi yetu viongozi, wanachama na mashabiki tunajua zaidi mpira kuliko tuliyemuamini tutataka afanye kile mbacho sisi tunahitaji.” alisema Dk Msolla.

Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni kocha alisema kwa muda mrefu walikuwa wanamtafuta kocha aina ya Kaze  na walipomkosa mara ya kwanza hawakukata tamaa.

 Alisema wamefanikiwa kumpata hivyo wampe uhuru wa kufanya kazi na  kikubwa wanatakiwa kusubiri matokeo ya uwanjani.

 “Kama tutaona matokeo yanayokuja hayaturidhishi tuna haki ya kumuhoji nini tatizo na sio kumpangia kikosi na hilo ni kama tunatimiza yale yote tuliyomuahidi.” alisema

Kaze wanatarajiwa kuonekana katika benchi la timu hiyo, wakati Yanga itakapocheza na Polisi Tanzania Alhamisi wiki hii, kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza wa msimu uliopita wa ligi hiyo, uliochezwa kwenye uwanja huo, timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3.

Baada ya mchezo wa Alhamisi, Kaze ataendelea na kibarua kizito cha kukiandaa kikosi chake ambao kitavaana na na watani wao Simba Novemba 7, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Mkapa.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *