Posted By Posted On

Katwila basi tena Mtibwa Sugar

NA ZAINAB IDDY

HATIMAYE  kocha wa timu ya Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, ameamua kubwaga manyanga kutokana na matokeo mabaya ya kikosi hicho Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika michezo sita  ya ligi hiyo ambayo, Mtibwa Sugar imecheza msimu huu, imeshinda mmoja ikitoka sare miwili na kupoteza mitatu huku ikiweka rekodi mbaya ya msimu iliyopita

Kutokana na sababu hiyo, jana Katwila alitangaza kuachia jukumu la kuifundisha timu hiyo, aliyerithi mikoba ya Meck Mexime ambaye kwa sasa anaifundisha Kagera Sugar.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana ndani ya Klabu ya Mtibwa Sugar jana, zilieleza kuwa, Katwila aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa uongozi juzi jioni.

Ilieleza kuwa jana  Katwila alikutana viongozi wa klabu hiyo  na kumbalia ombi lake la kujiuzulu kama kocha mkuu wa Mtibwa Sugar.

Katwila aliwasilisha  barua ya kujiuzulu kwa Bodi ya Mtibwa Sugar na jana uongozi kulazimika kukutana kwa dharura pamoja na kukaa chini na kocha na kuridhia uamuzi huo.

 Katika barua hiyo ya Katwila, alisema ameamua kujiweka pembeni kutokana na timu hiyo kukosa matokeo ya kuridhisha msimu huu,  lakini hata ule uliopita bado haukuwa mzuri kwake, hivyo kwa maslahi ya timu ameamua kukaa pembeni.”

BINGWA lilimtafuta Katibu wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur, alikiri kupokea barua ya Katwila na uongozi umebariki ombi lake kuachana na  timu hiyo.

Swabur alisema kwa sasa timu hiyo, itakuwa chini ya kocha wa kikosi cha vijana  Vicent Barnaba, hadi pale watapokamilisha mchakato wa kocha mkuu mpya.

Hata hivyo BINGWA likielekea kwenda mtamboni lilipata taarifa kuwa Katwila yupo mbioni kujiunga na timu ya Ihefu ambayo  kwa sasa haina kocha, baada ya Maka Mwalwisi kutimuliwa  kutokana na matokeo mabaya ya kikosi hicho katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *