Posted By Posted On

RC Mwanza alivyozidua usajili mbio za Rock City Marathon 2020:NA MWANDISHI WETU, MWANZA

JUZI Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alizindua rasmi usajili wa mbio za Rock City Marathon msimu wa 11, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kutoka Kanda Ziwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha maandalizi ya mbio.

Mbio za Rock City Marathon zinatarajiwa kufanyika Novemba 29, mwaka huu, eneo la  Rock City Mall jijini Mwanza.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa usajili wa mbio hizo iliyofanyika  jana jijini Mwanza, Mongella aliwaomba wadau mbalimbali wakiwamo washiriki na wadhamini kujitokeza kwa wingi ili kuunga mkono mbio hizo zenye agenda ya kutangaza utalii wa ndani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa na mkuu huyo wa mkoa pamoja na viongozi wengine waandamizi walijisajili kwa ajili kushiriki mbio hizo.

“Nasisitiza ushiriki wa wadau kutoka Kanda ya Ziwa hususani katika Mkoa wa Mwanza kwa sababu hizi ni mbio zetu haitapendeza sana kuona kwamba wadau wakuu wa mbio hizi wakiwamo wadhamini na hata washiriki wanatoka kwa wingi mikoa iliyo nje ya Kanda ya Ziwa.’’ anasema Mongella.

Ametoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali zikiwamo zile za watu binafsi kujitokeza ili kuongeza nguvu katika kufanikisha mbio hizo.

Hata hivyo, Mongella alizipongeza taasisi na mashirika mbalimbali ambayo tayari yamejitokeza kufanikisha mbio hizo  ikiwamo Kampuni za TIPER, Pepsi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Kampuni ya Ujenzi ya CRJE,  Pigeon Hotel, CF Hospital, Hospitali ya Bugando, Garda World, The Cask na Chuo cha SAUT Mwanza.

Mongella aliziagiza halmashauri za wilaya zote za mkoa huo kupitia maofisa michezo kuhakikisha wanahamasisha usajili wa washiriki wengi iwezekanavyo ili mkoa huo uweze kupata wawakilishi wa kutosha kiasi cha kuakisi uenyeji wao katika kuandaa mbio hizo.

“Mkoa wa Mwanza una historia ya kutoa wanariadha wakubwa walioipatia nchi hii heshima kubwa katika mchezo wa riadha akiwamo Suleimani Nyambui.

Tunahitaji kuendeleza heshima hiyo kupitia mbio hizi, hivyo tusimame wote pamoja kufanikisha hili. Washiriki wajitokeze kwa wingi na pia wadhamini wajitokeze kwa wingi,’’ ameongeza.

Mbali na usajili huo, Mratibu wa mbio hizo, Kasara Naftal alimkabidhi mkuu huyo wa mkoa moja ya fulana maalum zitakazotumika katika mbio hizo katika msimu huu.

Naftal alibainisha kuwa tayari maandalizi muhimu yameshafanyika ikiwamo suala zima la fulana za washiriki pamoja na medali huku akitaja mbio zitakazohusishwa ni  kilomita 21, kilomita 10 na kilometa tano.

Anasema usajili wa mbio hizo tayari umekwishaanza kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya mbio hizo pamoja na usajili wa kawaida kupitia vituo mbalimbali vilivyopo mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dodoma, Arusha huku mikoa zaidi ikiendelea kuongezwa.

“Usajili unaendelea vizuri na mwitikio wa washiriki ni mkubwa. Lengo ni kukimbiza washiriki  wasiopungua 3000 yakiwamo makundi yote yaani wakimbiaji wa mbio za ushindani (Elite runners), washiriki wa mbio za kujifurahisha (Fun run) pamoja na wanafunzi.” anasema Naftal.

 “Kuhusu zawadi,  pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. mil. 2 kila mmoja, wakati washindi wa pili akizawadiwa sh.mil,  1.3, washindi wa tatu Sh. 700,000 huku washindi wanne hadi kumi nao pia wakiibuka na zawadi  za medali na pesa taslimu.’’

“Kwa upande wa mbio za kilomita 10 hatutakuwa na zawadi za fedha taslimu isipokuwa washiriki watajipatia medali na fulana.

Kuhusu mbio za kilomita tano ambazo zitahusisha washiriki kutoka mashirika na taasisi mbalimbali  sambamba na washiriki wenye ualbino zawadi za fedha taslimu zitatolewa kwa washindi watatu wenye ualbino pekee.’’ anasema.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *