Posted By Posted On

SVEN AJA NA USHINDI KIMBUNGA

NA ASHA KIGUNDULA

KOCHA wa Simba, Sven Vanderbroeck, amesema  licha  kupata upinzani mkali kutoka kwa Yanga na Azam katika vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ana amini kikosi chake kitaendelea kupata ushindi wa kimbunga utakaobeba kutetea lao kwa mara ya nne mfululizo

Kwa sasa Simba wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi 13, sawa na Yanga, lakini wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa huku Azam wakiwa kileleni kwa pointi 18.

Kutokana na matokeo hayo, Vanderbroeck alisema jijini  Dar es Salaam juzi, wakati Simba ikicheza na Mlandege ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuwa wanajipanga vizuri kuhakikisha anapata ushindi wa mabao mengi Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo huo, Simba ilishinda mabao 3-1 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons utakaochezwa Alhamisi wiki hii kwenye  Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Vanderbroeck alisema kuwa, ana matumaini makubwa kikosi chake kitaendelea kupata ushindi sambamba na idadi kubwa ya mabao ambayo yatakuja kuwa na faida mwishoni mwa msimu huu.

Kocha huyo alisema kuwa, kutokana na ubora wa safu yake ya ushambuliaji, inayoongozwa na Middie Kagaere, John Bocco na Chris Muguli ana uhakika wa kufunga bao zaidi ya moja katika kila mchezo wa ligi hiyo.

Katika hatua nyingine, Vanderbroeck alisema kuwa, kikosi chake kitaondoka leo kwenda mkoani Rukwa, tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi Tanzania Prisons.

Vanderbroeck alisema kuwa wanaifuata Tanzania Prisons wakiwa na tahadhari kubwa, kwani wanaheshimu wapinzani kwa kuwa ni moja ya timu imara.

 “Kila timu imejipanga kushinda mechi zake inazocheza, na sisi tumejipanga si kushinda tu, bali kushinda idadi kubwa ya mabao ambayo  yatatusaidia kutuweka mahali sahihi,”alisema Vanderbroeck

Hadi  sasa Simba wanacheza michezo sita  tangu ligi hiyo ilipoanza Septemba 7, mwaka huu, ikishinda mitano na sare moja, ikiwa imefanikiwa kufunga mabao 14.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *