Posted By Posted On

MAZOEZI YANGA YANALETA RAHA AISEE

Msomaji wa Yanganews Blog:Sharti la kwanza la kocha mpya wa Yanga, Cedrick Kaze mazoezini ni kwamba unagusa mpira mara moja unaachia kwa mwenzio tena kwa kasi.

Na kwa mujibu wa Kaze mzuka ni mkubwa kwa wachezaji, viongozi na benchi la ufundi la Yanga ikiwa ni siku chache tu kabla ya kukipiga na Polisi Tanzania Alhamisi Jijini Dar es Salaam.

Kwa mara ya kwanza Kaze alianza kufundisha mbinu Jumapili ikiwa ni siku yake ya pili tangu aanze kukinoa kikosi hicho. Katika mazoezi hayo ambayo yalianza saa 10:30 jioni walikuwepo baadhi ya viongozi akiwamo Mshindo Msolla ambaye ni Mwenyekiti wa klabu hiyo pamoja na Mshauri wa uongozi, Senzo Mazingiza.

Aliyeanza kusimamia mazoezi hayo, alikuwa Elieneza Nsanganzelu ambaye anatajwa kama kocha wa viungo, alianza na mazoezi mepesi ambayo yalikuwa yakilenga kuwanyoosha miili wachezaji kabla ya kuingia awamu nyingine ya mazoezi ya viungo.

Awamu nyingine ilionekana kulenga kuifanya miili kuwa tayari kwa programu za kiufundi za Kaze, wachezaji wa Yanga walikuwa wakikimbia mbio fupi kwa karibu dakika 10 na miili yao ilipoonekana kupata joto ndipo walipopewa dakika mbili za kunywa maji kabla ya kuingia kwenye awamu ya tatu ya mazoezi.

Kaze ndiye aliyehusika kwenye awamu hiyo, aliwagawa kwa makundi wachezaji wake huku yakitengwa magoli mawili moja alisimama Metacha Mnata na jingine Farouk Shikhalo na kuna muda walikuwa wakibadilisha na Ramadhan Kabwili, zoezi hilo alikuwa akijaribu kutengeza muundo wa kufanya mashambulizi.

Zilikuwa zikipigwa pasi fupi fupi za haraka, walianza kwa kwenda taratibu, zoezi lilipoeleweka ndipo muundo ukabadilika na kuanza kufanyika kwa haraka, zilikuwa zikipigwa sambusa za hapa na pale huku kila mchezaji akitakiwa kufanya umaliziaji.

Haruna Niyonzima, Feisal Salum, Mukoko Tonombe, Deus Kaseke, Wazir Junior walikuwa miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wakimfurahisha kocha, walikuwa wakigusa mpira kwa haraka na kuwa kwenye nafasi kisha kuwa na umaliziaji mzuri.

Pia katika mazoezi hayo yakiwa yanaendelea, kiungo Abdulaziz Makame alikuwa akifanya programu ya peke yake akiwa anasimamiwa na daktari wa viungo.

Alikuwa amemfunga kamba aina ya mpira kiungo huyo kisha alimtaka awe anakimbia kwa nguvu na yeye anamvuta, zoezi ambalo lilionekana kuwa zuri kwa kiungo huyo.

Baada ya mazoezi kumalizika, chanzo chetu ilizungumza na kocha Kaze na akasema; “Kitu kikubwa na kizuri ni kwamba wachezaji wanafanya mazoezi kwa hali ya juu, timu iko vizuri kwa wachezaji wote lakini wapo ambao wanaumwa kama Carlinhos, Makame, Fahad Fuad ambao wameshindwa kufanya mazoezi ya pamoja na wenzao leo, lakini upande wa Balama yeye bado na majeraha yake ni ya muda mrefu hiyo inajulikana, hii inanipa picha nzuri ya kikosi changu.”

Alisema yeye ni muumini wa soka la haraka kwenda langoni kwa wapinzani kwani anaamini akifanya hivyo ndio atapata magoli mengi zaidi kuliko kukaa nyuma.

“Ni falsafa yangu ya mpira hii, mpinzani wangu anaweza kufanya makosa na sisi tukatumia mbinu hii, tunatakiwa tuingie ndani ya boksi lakini pia tuwe na uwezo wa kupiga mashuti nje ya boksi kwa sababu muda mwingine timu tunazokutana nazo tunaweza tusiingie ndani ya boksi lakini tukatumia njia ya kupiga mashuti nje ya boksi.”

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *