Posted By Posted On

Rogers mwanamuziki anayevutiwa na Marijani

NA JEREMIA ERNEST

BONGO Star Search (BSS), ni shindano lililofanikiwa kuibua vipaji vingi vya wanamuziki wa Tanzania ambao miongoni mwao kwa sasa wanafanya vizuri.

Wakali kama Rogers Lucas, Baby Madaha, Kayumba, Jumanne Idd, Peter Msechu, Haji Ramadhan, Kala Jeremiah, Walter Chilambo na Mesh Amazing ni zao la shindano hilo.

Katika safu hii leo tunakuwa na Rogers Lucas ambaye ni mmoja wa wasanii aliyeibuliwa kimuziki na shindano hilo, linaloendeshwa na Kampuni Benchmark Production chini ya mkurugenzi wake, Rita Paulsen.

Rogers kabila lake ni Muha kutoka Mkoa wa Kigoma, anasema licha ya kuwa na umaarufu kwenye muziki, lakini hapendi kuweka wazi maisha yake binafsi kwa sababu hayaweza kumsaidia shabiki wake.

Mwanamuziki huyo ambaye ni mtaalamu wa kuimba na kupiga gitaa, anasema alianza kuimba  tangu akiwa umri mdogo kanisani chini ya mwalimu aliyemtaja kwa jina la Gelly na alipofikia mtu mzima alipokea ushauri wa kuingia kwenye muziki kutoka kwa baba, mama na rafiki zake.

Anasema yeye ni shabiki na mfuatilia mzuri wa muziki mahadhi ya RnB, Soul, Reggae na Pop, huku akivutiwa na muziki wa Marijani Rajab, Stara Thomas na Banana Zorro.

Mwanamuziki huyo anasema Bongo Star Search (BSS), ilimtambulisha kwa mashabiki wake mwaka 2007 hadi 2008, ambapo alikuwa mshindi wa pili.

“Nilifahamika baada ya kushiriki shindano la BSS mara mbili katika msimu wa pili na wa tatu ambapo kote nilikuwa mshindi wa pili,” anasema.

Rogers anajivutia kutumia nyimbo zake katika shindano hilo hasa wimbo, Rudi ambao ulimpa umaarufu na kubeba jina la albamu yake ya kwanza.

ATOA NENO KUHUSU BSS

Mwanamuziki huyo anasema anaamini mashabiki walimpigia kura za kutosha na alipaswa kuwa mshindi wa kwanza, lakini alitangazwa kama mshindi wa pili.

“Nilitangazwa mshindi wa pili wakati nilitakiwa kuwa wa kwanza, niligundua hilo baada ya kupigiwa kura na watu wengi walikuwa wakifuatilia,” anasema Rogers.

 Anasema hana maana kwamba majaji walimwonea ila kwa namna fulani hawakuwatendea haki mashabiki waliompigia kura wakitarajia kuwa atakuwa mshindi.

“Kwangu nafasi hazikuwa na maana hata wangenipa ya tano, sababu lengo lilikuwa kuwaonesha watu kipaji changu, kunikubali kwao kwa wingi kulifanya nifurahi zaidi ya kupewa nafasi ya pili,” anasema.

Kwanini hasikiki tena? Anasema hajawahi kuwa kimya katika muziki kwa sababu ameendelea kuwa bora zaidi siku hadi siku, isipokuwa amekuwa na changamoto kadhaa.

“Mimi ni muziki na muziki ni maisha yangu, ukiacha matatizo ya mfumo wa soko nchini, kwetu changamoto kubwa ipo katika kupata watu sahihi wa kushirikiana nao katika kupiga hatua mbele zaidi,” anasema Rogers.

Rogers anasema akisema mfumo anamaanisha kila kitu kinachohusu biashara ya muziki wasanii wazuri wanakwama

YUPO WAPI?

Anasema kwa sasa anaishi jijini Dar es Salaam anaendelea kufanya kazi za muziki ila akipata shughuli nyingine anafanya pia.

Kwa sasa bado hajawa tayari kuweka mipango yake ya kuendeleza muziki ila si muda mrefu atarudi na mashabiki waje wakae tayari kumpokea.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *