Posted By Posted On

KAZE WALA HANA HOFU, MECHI LIGI KUU DHIDI POLISI TANZANIA

Msomaji wa Yanganews Blog;Mashabiki wa Yanga wanahesabu saa tu kabla ya kutimba Uwanja wa Uhuru kucheki shoo ya kwanza kwa timu, ikiwa chini ya Kocha Cedric Kaze itakapoivaa Polisi Tanzania katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu, huku kocha huyo mpya akitamba kila kwake kipo freshi kilichobaki shoo tu.

Yanga ya Kaze. Kocha huyo aliyesainishwa mkataba wa miaka miwili kuchukua nafasi ya Zlatko Krmpotic kutoka Serbia aliyetumuliwa licha ya kuiongoza timu hiyo kwenye mechi tano za Ligi Kuu Bara bila kupoteza na kuiacha na alama 13 kwa kushinda mechi nne na kutoka sare moja, leo atakuwa na kibarua cha kuanzia pale alipoishia mtangulizi wake.

Kocha huyo kutoka Burundi anayesifika kwa falsafa ya soka la pasi nyingi na kushambulia mwanzo mwisho, juzi na jana alikuwa akiwanoa vijana wake kwa mara ya mwisho kabla ya kuivaa Polisi huku akisisitiza tayari ameshapata mwanga wa kikosi chake cha kwanza na mbinu mpya za kuingia nazo.

Tangu ujio wake Jangwani, Kaze ameleta kicheko kwa wachezaji, viongozi na mashabiki kwa kuamini kuwa lile soka tamu lililopotea kwa timu yao chini ya Zlatko linarudi upya kwenye mechi yao leo, huku mwenyewe akisisitiza hana hofu yoyote kwa vile alishasoma mchezo kabla ya kuja nchini.

Juzi kabla ya kuanza kwa mazoezi ya timu yake kwenye kambi yao Kigamboni, kocha huyo alianza kufanya mazungumzo na wachezaji kadhaa, akiwapa maelekezo ya nini wanatakiwa kufanya na hata baada ya kumaliza akawaweka kikao.

Alianza kuzungumza na mshambuliaji Wazir Junior kwa muda wa dakika 3 kisha akafuata Haruna Niyonzima, lakini baada ya mazoezi aliwaita pembeni Deus Kaseke, Lamine Moro na Zawadi Mauya.

Alipoulizwa na chanzo chetu alifafanua anafanya mazungumzo na wachezaji kabla ya mazoezi, sababu ya kwanza aliitaja kwamba ni kuifanya timu iwe kitu kimoja na kila mchezaji ajione ana umuhimu mkubwa Yanga.

Juu ya kikosi cha kwanza alisema kwa muda aliokaa na timu hiyo, tayari ameanza kupata mwelekeo wa kikosi cha kwanza, kupitia mazoezi yanayoendelea na matunda yake yataanzia kwa Polisi

“Naamini kadri muda unavyoendelea ndivyo kikosi changu kitazidi kuwa bora.”

Kocha Kaze alisisitiza anapenda kuona wachezaji wake wanacheza mpira wa kasi ambao utakuwa unazalisha mabao mengi.

“Napenda kuona timu inacheza kwa kujiamini na mpira wa kasi ambao utatuletea mabao mengi, nimeangalia kikosi naona linawezekana na lipo ndani ya uwezo wao,” alisema kaze na kuongeza anaiheshimu Polisi Tanzania, lakini anaamini ana kikosi kinachojua kinatakiwa kufanya nini katika mchezo huo, huku akimkosa kiungo mshambuliaji Carlinhos aliye majeruhi.

“Kuhusu Uwanja wa Uhuru, siwezi kuulalamikia kwasababu zinacheza timu mbili, kikubwa ni wachezaji kuwa tayari kwenda kuipambania timu yetu, hilo ndilo jambo la msingi zaidi kwasasa.”

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *