Posted By Posted On

Kigogo Yanga amtabiria JPM

NA MWANDISHI WETU MMOJA wa vigogo wa Yanga, Athuman Kihamia ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, amemtabiria ushindi wa kishindo mgombea uraia kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli (JPM) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu. Akizungumza na BINGWA jana kutoka Rombo, Kihamia ambaye ni miongoni mwa wanachama maarufu wa Yanga, aliyesaidia kulipaisha tawi la klabu hiyo la Kariakoo, Dar es Salaam, alisema kuna mambo mengi yanayombeba JPM kuelekea uchaguzi huo. Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni kuwajali watanzania hasa wanyonge katika huduma za msingi kama elimu, huduma za afya, maji, umeme, ujenzi wa miundombinu kama barabara na nyinginezo. Alisema kuwa JPM amefanya mengi mazuri ndani ya muda mfupi, akiamini iwapo atadumu madarakani kwa miaka mingine mitano, Tanzania itakuwa moja ya nchi za kutolewa mfano duniani. “Kuna mengi sana amefanya Rais Magufuli ndani ya muda mfupi… ukiachana na suala la elimu ya msingi bure, ujenzi wa barabara, reli, ununuzi wa ndege na miradi mingine mingi, pia amerejesha nidhamu ya kazi kwa watendaji. “Kwa sasa watendaji wamekuwa na nidhamu ya kazi, hakuna ujanja ujanja kama ilivyokuwa zamani. Kwa mtanzania mwenye mapenzi ya kweli na nchi yake, hawezi kuacha kumchagua Magufuli kuwa rais katika uchaguzi wa Oktoba 28,” alisema. Alisema hata wanamichezo, wanalo la kujivunia kwa JPM kwani amefanya makubwa, ikiwamo ahadi yake ya kujenga uwanja wa kisasa wa michezo jijini Dodoma. Kihamia aliwataka wapenzi wa Yanga na watanzania kwa ujumla, kumpa kura za ndiyo Rais Magufuli, akiamini atawafanyia makubwa zaidi miaka yake mitano ijayo ya uongozi.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *