Posted By Posted On

MAMBO YAMEANZA KUIVA, MCHAKATO MABADILIKO YANGA

Msomaji wa Yanganews Blog:Mabosi wa Bodi ya Ligi Kuu Hispania (La Liga) wametangaza neema kwa mashabiki na wanachama wa Yanga baada ya kufichua awamu ya kwanza ya mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo yamekamilika na kinachofuata ni utekelezaji wake.

Akizungumza jijini jana, Mwakilishi wa La Liga, Alvaro Paya alisema awamu hiyo ya kwanza ilijikita katika masuala mawili yaliyofanyiwa tathmini ya kina na kisha kuwekwa katika ripoti iliyoshiba itakayokabidhiwa kwa uongozi wa Yanga.

“Mambo mawili makubwa tuliyokuwa tukiyafanyia kazi katika kipindi cha takribani miezi mitano tangu Mei tuliposaini makubaliano na Yanga na ushiriki wa mashabiki na pia mfumo wa uendeshaji wa klabu,” alisema Paya na kuongeza;

“Kazi hiyo imefanyika kwa umakini na weledi wa hali ya juu kwa kufanya tathmini klabuni na sasa imekamilika ambapo ripoti tayari tumeshaiandaa na wiki ijayo tutaikabidhi rasmi.”

Mwakilishi huyo alisema; “Kiujumla ripoti ina kurasa takribani 400 ambapo wiki ijayo tutaikabidhi na tutaichambua kwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga ambaye naye ataiwasilisha kwa klabu. Kimsingi ripoti imeelezea na kufafanua mambo muhimu ambayo yakitekelezwa, Yanga itapiga hatua na kupata mafanikio makubwa.”

Paya alisema katika muda wote ambao La Liga imekuwa ikifanya kazi na Yanga, imenufaika na kujifunza mengi ikiwemo namna Yanga ilivyo na mtaji mkubwa wa mashabiki katika kila pembe ya nchi ambao wanaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo ya klabu hiyo.

Alisema ushirikiano baina yao na Yanga umekuwa na mafanikio makubwa kwa kila upande na anaamini utaleta tija kubwa siku za usoni.

Mei 31 mwaka huu, uongozi wa Yanga ulisaini mkataba wa miaka mitatu na La Liga ili iwaongoze katika mchakato wamabadiliko ya mfumo wa uendeshaji.

Mkataba huo una awamu nne, ya kwanza ikiwa ni hii iliyokamilika ambayo ina thamani ya kiasi cha Euro 80,000 (zaidi ya Sh205 milioni), gharama ambazo zinalipwa na kampuni ya GSM.

Maeneo makubwa yaliyoainishwa na kupangwa kufanyiwa kazi katika mkataba huo baina ya Yanga na La Liga ni maendeleo katika nyanja za ufundi, masoko pamoja na uongozi.

,,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *