Posted By Posted On

KMC kumaliza hasira kwa Gwambina

NA WINFRIDA MTOI

BAADA ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Yanga, kocha msaidizi wa timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC), Habib Kondo, amesema watahamishia hasira kwa Gwambina  wanaotarajia kukutana Ijumaa wiki hii, ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Gwambina, Misungwi, mkoani Mwanza.

KMC walipoteza mchezo huo, uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Akizungumza na BINGWA kwa simu kutoka Mwanza jana, Kondo, alisema walifanya makosa katika mechi iliyopita na kusababisha  kufungwa bao la pili, lakini walicheza vizuri.

Kondo alisema ligi ni kama mbio za marathoni bado hawajakata tamaa wanaamini watarudi katika nafasi yao kutokana na michezo iliyobaki ni mingi kuliko waliyocheza.

“Tumepoteza mchezo tunajipanga na mechi ijayo, tutakutana na Gwambina ugenini, nitatumia  siku hizi chache kufanya marekebisho ya makosa yaliyojitokeza.

“Hatuwezi kusema tumepotea kwa kufungwa, hii ni ligi ina changamoto zake na pia ni kama mbio za marathoni  naamini KMC itafanikiwa malengo yake,” alisema Kondo.

KMC ambayo ilianza kwa kasi ligi hiyo na kuwa kinara kwa muda, kwa sasa inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 11, baada ya kucheza mechi nane, imeshinda tatu, sare mbili na kupoteza tatu.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *