Posted By Posted On

Mtibwa yaitungua Azam Jamhuri, Prisons yazidi kupeta

NA GLORY MLAY

TIMU ya Azam FC imepoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Pamoja na kipigo hicho, Azam inaendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi nane, ikishinda saba, ikifuatiwa na Yanga walioshuka dimbani ma ra saba na kujikusanyia pointi 19.

Kwa upande wao, ushindi wa jana umeiwezesha Mtibwa Sugar kupanda hadi nafasi ya 10 kutoka ya 15.

Bao la Mtibwa Sugar lilifungwa na Jafary Kibaya dakika ya 62 na kudumu hadi dakika 90 za mchezo huo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit, alisema kuwa ulikuwa mgumu na wa ushindani, akisisitiza wamekubali matokeo, hivyo wanajipanga kwa ajili ya mchezo mwingine unaofuata.

“Haukuwa mchezo wetu, tumekwama leo na kupoteza pointi tatu, tunajipanga kwa ajili ya mechi zetu zijazo, nadhani mwalimu kaona kasoro, hivyo atazifanyia kazi ili kupata ushindi wa pointi tatu,” alisema.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, amesema mchezo ulikuwa wa ushindani na kwamba walicheza kwa akili kutokana na ubora wa wapinzani wao.

“Walikuwa wanawaonea wadogo hao Azam FC, leo wamekutana na timu kubwa, tukawatuliza,” alisema.

Katika mchezo mwingine, timu ya Tanzania Prisonns imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Ushindi huo wa pili mfululizo, umeiwezesha Prisons kupanda hadi nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 12, sawa na Dodoma Jiji waliopo juu yao kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *