Posted By Posted On

KAZE AWAFUNGIA KAZI MASTRAIKA

NA MOHAMED KASSARA LICHA ya kuiongoza Yanga kushinda michezo miwili mfululizo, kocha wa kikosi hicho, Cedric Kaze, amesema haridhishwi na ushindi mwembamba wanaoupata, huku akiweka wazi kuwa ameanza kuwafungia kazi washambuliaji wake ili watupie mabao ya kutosha katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara. Kaze ambaye alirithi mikoba ya Zlatko Krmpotic hivi karibuni, amekiongoza kikosi
The post KAZE AWAFUNGIA KAZI MASTRAIKA appeared first on Gazeti la Dimba.,

NA MOHAMED KASSARA

LICHA ya kuiongoza Yanga kushinda michezo miwili mfululizo, kocha wa kikosi hicho, Cedric Kaze, amesema haridhishwi na ushindi mwembamba wanaoupata, huku akiweka wazi kuwa ameanza kuwafungia kazi washambuliaji wake ili watupie mabao ya kutosha katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara.

Kaze ambaye alirithi mikoba ya Zlatko Krmpotic hivi karibuni, amekiongoza kikosi hicho katika michezo miwili iliyopita na kuvua pointi zote sita, akianza kuvuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, kabla ya kuichapa KMC mabao 2-1.

Hata hivyo, Mrundi huyo amesema bado hafurahishwi na aina ya ushindi wanaopata akidai washambuliaji wake wanatakiwa kuongeza ubunifu, kasi na maarifa ili kufunga mabao mengi zaidi kulingana na nafasi wanazotengeneza.

Kaze amewafungia kazi washambuliaji wake, Michael Sarpong, Yacouba Sogne, Ditram Nchimbi na Waziri Junior na kuwataka kuhakikisha wanafunga mabao ili kuipa timu hiyo ushindi mnono.

Hatua hiyo imetokana na kasi duni ya upachikaji mabao ya washambuliaji wa timu hiyo ambapo hadi sasa wamefunga mabao matatu tu kati ya 10 yaliyofungwa na kikosi hicho hadi sasa.

Sarpong amecheza dakika 458, sawa na mechi tano na kufunga bao moja, Sogne amecheza dakika 299, sawa na mechi mbili na kufunga bao moja, Waziri Jr amecheza mchezo mmoja na kufunga idadi kama hiyo, huku Nchimbi akichezea dakika 76 bila kufunga.

Kinara wa mabao ndani ya kikosi hicho ni mlinzi wa kati ambaye pia ni nahodha, Lamine Moro, mwenye mabao mawili sawa na kiungo, Mukoko Tonombe. Mabao mengine ya Yanga yamefungwa na Carlos Carlinhos, Tuisila Kisinda na Haruna Niyonzima, ambao kila mmoja ametikisa nyavu mara moja.

Baada ya mechi ya KMC, Kaze alisikika akisema anafurahia kuona kikosi chake kinaendelea kupata ushindi, lakini akiweka wazi kuwa mabao yanayofungwa bado ni kiduchu ukilinganisha na mahitaji.

Alisema licha ya timu kuanza kuonyesha mabadiliko hususan ikiwa na mpira ngumu kuupoteza na kucheza katika eneo la mpinzani muda wote, lakini bado kasi ya upachikaji mabao imekuwa kikwazo kwa timu yake.

“Nimekaa na timu muda mchache, hivyo kuna vitu vya kuboresha ili kuhakikisha timu inacheza soka lile ninalolitaka mimi la pasi nyingi na kasi.

“Hivi sasa nazifanyia kazi baadhi ya sehemu zenye upungufu ikiwemo safu ya ushambuliaji ambayo yenyewe inaonekana kushindwa kutumia nafasi nyingi zinazopatikana na hiyo ni kutokana na timu kutokuwa na muunganiko mzuri tunapofika langoni mwa mpinzani,” alisema Kaze.

Kocha huyo pia alisema amesikia kilio cha mashabiki wa timu hiyo wakitaka kuiona timu yao inatwaa ubingwa msimu huu baada ya kuukosa kwa vipindi vitatu na kudai kwamba anatarajia kuwapa furaha hiyo.

Mpaka sasa Yanga ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na jumla ya pointi 19, baada ya kucheza michezo saba, Azam FC iliyocheza minane inaongoza ikiwa na jumla ya pointi 21.

The post KAZE AWAFUNGIA KAZI MASTRAIKA appeared first on Gazeti la Dimba.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *