Posted By Posted On

Janja yenu kwishnei

Simba ajivunia kubaini mapema na kuwasambaratisha ‘wachawi’ wao

Wasema sasa ni mwendo mdundo, kila ajaye mbele yao ni dozi tu

NA MICHAEL MAURUS

KLABU ya Simba imesema kuwa kwa sasa hakuna cha kuwazuia kushinda mechi zao zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine iliyopo mbele yao, kwani washatibu tatizo lililokuwa likiwatesa.

Simba ilipoteza mecghi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kuzinduka Jumamosi iliyopita kwa kuichapa Mwadui FC mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kabla ya ushindi huo mnono, Simba ilifungwa bao 1-0 na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, Rukwa, kabla ya kupokea kipigo kama hicho kutoka kwa Ruvu Shooting, Dimba la Uhuru, Dar es Salaam.

Baada ya vipigo hivyo, uongozi wa Simba ulikaa chini na kutafakari kulikoni ndipo walipobaini chanzo cha tatizo na kukipatia ufumbuzi.

Moja ya hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Simba, ilikuwa ni kuwatimua baadhi ya watendaji wao, lakini pia kukutana na wachezaji na kuzungumza nao.

Katika kinachoonyesha kuwa hatua hizo mbili zuilizochukuliwa na uongozi zimezaa matunda, juzi Jumamosi Wekundu wa Msimbazi hao waliwapa raha mashabiki na wanachama wao kwa kupata ushindi huo mnono wa mabao 5-0.

Akizungumza na BINGWA wikiendi iliyopita, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Barbara Gonzalez, alisema kuwa baada ya hatua walizochukua, kwa sasa hali ni shwari Msimbazi, wakiamini hakuna mechi nyingine watakayopoteza.

Alisema ukiachana na hatua ya kuwafukuza baadhi ya wafanyakazi wao, lakini kitendo cha kukutana na wachezaji na kuzungumza nao, walibaini mambo kadha wa kadha yaliyochangia kupoteza kwao mechi mbili mfululizo na kuyapatia ufumbuzi.

“Unaapoona sehemu kuna shida, lazima kuwe na sababu. Kwa kikosi chetu cha sasa si cha kupoteza mechi kirahisi, tena mechi mbili mfululizo. Tulijua lazima kutakuwa na sababu na kweli ilikuwa hivyo.

“Tukaona tufanye uamuzi wa kuwatoa baadhi ya watu, halafu tukaona ni vema kukutana na wachezaji. Tulizungumza nao na kuwakumbusha wajibu wao na msimamo wetu kama klabu juu ya mambo mbalimbali, ikiwamo suala la kocha.

“Kwa pamoja walituelewa na kuahidi kuipigania timu kupata ushindi katika kila mechi. Tunashukuru mchezo wetu wa kwanza toka tulipokutana nao, tumepata ushindi mnono, bila shaka tutaendelea hivi hadi mwisho wa ligi,” alisema Barbara.

Alisema kuwa wapenzi wa Simba kwa sasa hawana haja ya kuwa na presha zaidi ya kujitokeza kwa wingi uwanjani kwani ile mianya ya hujuma dhidi ya kikosi chao, haipo tena.

“Mashabiki waipe sapoti timu, bila wao Simba haiwezi kufika popote. Klabu hii imejengwa katika msingi wa umoja na mshikamano kuanzia kwa mashabiki, wanachama, wachezaji hadi viongozi,” alisema.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba ipo nafasi ya tatu, ikiwa imejikusanyia pointi 16 kutokana na mechi nane, huku Azam iliyocheza mechi tisa, ikiongoza na pointi 22 sawa na Yanga iliyopo nyuma yao, lakini Wanajangwani hao wakishuka dimbani mara nane.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *