Posted By Posted On

SIMBA JEURI

Michael Maurus

SIMBA wana dharau aisee asikwambie mtu. Pamoja na kasi ya Yanga katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara, Wekundu wa Msimbazi hao wamesema kuwa kamwe hawaumizwi vichwa na Wanajangwani hao kwani wanafahamu wapi pa kuwakamata.

Wakiwa wanashuka dimbani kesho kukipiga na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara, Simba wamekuwa wakifanya maandalizi ya kuua ndege wawili kwa jiwe moja, yaani kushinda mechi zao zote mbili za wiki hii.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Simba wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 16 baada ya kucheza mechi nane, huku Yanga wakiwa juu yao na pointi zao 22, nao wakishuka dimbani mara nane.

Azam wenye pointi 22 sawa na Yanga, wapo kileleni wakibebwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, lakini wao wakiwa wamecheza mechi tisa.

Pamoja na pengo la pointi sita baina yao na Yanga, Simba wameendelea kutamba kutetea ubingwa wao wa ligi hiyo, kwa kulitwaa taji kwa msimu wa nne mfululizo.

Akizungumza na BINGWA jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema kuwa kwa sasa kikosi chao kipo sawasawa, hakuna tatizo lolote linaloweza kuwazuia kuvuna pointi zote tatu kesho na mechi zijazo.

Alisema walipoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara kutokana na mambo madogo madogo yaliyokuwa ndani ya kikosi chao ambayo kwa sasa wameshafanyia kazi, hivyo hawana sababu ya kupoteza pointi kwa Kagera Sugar zaidi ya kuibuna na ushindi mnono kama ilivyokuwa mwishoni mwa wiki dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Uhuru waliposhinda mabao 5-0.

“Kuna hatua kadhaa tumechukua ili kurejesha morali ya ushindi kwa timu yetu na sasa hali ni shwari, hivyo ushindi ni lazima keshokutwa (kesho),” alisema.

Alisema kuwa wamezungumza na wachezaji wao na kubaini baadhi ya mambo yaliyokuwa yakiwakwanza ambayo wameyafanyia kazi na vijana wao hao, wamewaahidi kuendelea kushusha vipigo VPL.

 “Kulikuwa na shida, tukaona ni vema pia tukazungumza na wachezaji. Haiwezekani timu yenye wachezaji wa kiwango cha juu kama Simba, ipoteze mechi mbili mfululizo, tena hadi nyumbani!

“Baada ya kukaa nao, tukabaini baadhi ya mambo ambayo tumeshayamaliza na kilichobaki kwa wachezaji ni kurejesha matumaini ya mashabiki wa Simba kwa kupata ushindi mzuri.

“Ninachopenda kusema kwa sasa hali ni shwari ndani ya kikosi cha Simba, tunatarajia hatutapoteza tena mchezo wowote wa ligi,” alitamba Barbara.

Aliwataka wapenzi wa Simba kuendelea kuiunga mkono timu yao kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho ili kuzidi kuwapa mzuka wachezaji na kucheza kwa uwezo wao wote kuipa timu ushindi mnono kama walivyofanya dhidi ya Mwadui.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, alisema kuwa vijana wake wapo tayari kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo kwa kushinda kesho.

Alisema kuwa katika kikosi chake cha kesho, ataendelea kufanya mabadiliko ya wachezaji kama sehemu ya kuandaa jeshi la kuiangamiza Yanga Jumamosi.

Katika hatua nyingine, mmoja wa viongozi wa juu wa Simba, amesema kuwa tayari wameshamaliza kazi kuelekea mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Yanga, akiahidi ushindi mnono.

“Awali tulikuwa na presha, lakini tukagundua kuna watu wetu wawili ambao tukiwatumia vizuri, Yanga wanakufa, tena nyingi tu. Tumewasiliana na watu hao na kwa sasa kila kitu kipo sawa,” alitamba kigogo huyo aliyekuwa akiunda kundi la Friends of Simba.

Alipotakiwa kuwataja watu wao hao, alisema: “Yaani niwataje halafu mpango wetu uvurugike! Siwezi kusema kama wapo ndani ya kikosi cha Yanga au ni ndani ya timu yetu, ninachokudokezea ni kwamba Yanga hawana pa kutokea Jumamosi, tayari tumeshamaliza mchezo, kilichobaki ni kwa kocha na wachezaji kutekeleza majukumu yao uwanjani kuwapa raha Wanasimba.”

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *