Posted By Posted On

Zahera azoa zaidi ya mil 100/- Yanga

WINFRIDA MTOI

KLABU ya Yanga imemlipa kocha wake wa zamani, Mwinyi Zahera, malimbikizo ya fedha alivyokuwa anadai ambazo ni dola za Kimarekani 41,000, sawa na shilingi 121,998,000 za Kitanzania.

Zahera aliyeachana na Yanga msimu uliopita, amelipwa fedha hizo hivi karibuni baada ya kushinda kesi aliyopeleka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Akizungumza jana wakati alipotembelea kampuni ya New Habar(2006), wachapishaji wa magazeti ya MTANZANIA, BINGWA, DIMBA na RAI, msimamizi wa Zahera, Yasmin Razak, alithibitisha kuwa tayari kocha huyo amemalizana na Yanga.

Alisema kwa muda mrefu walikuwa wakishughulikia suala hilo na mwanasheria kutoka kampuni ya Livida Sports ya nchini Uingereza.

“Zahera ameshamalizana na Yanga, amelipwa fedha zake alizokuwa anadai ambazo ni dola 41,000, hakuna tena deni,” alisema.

Yasmin alieza kuwa si meneja wa Zahera, lakini alipata malalamiko yake na kumsaidia kumuunganisha na kampuni hiyo inayoshughulikia wanamichezo wengi kisheria.

Alifafanua kuwa kulikuwepo na changamoto kwa sababu imechukua miezi kadhaa, lakini kilichomfanya kocha huyo kufanikiwa kupata haki yake ni aina ya watu aliotumia kufikisha suala lake FIFA.

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *