Posted By Posted On

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi ameiagiza Idara ya Maen…

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo kukutana na Wadau wa sekta hiyo wakiwemo Mashirikisho na Vyama vya Michezo ili kubadilishana utaalamu wa namna ya kuendesha michezo pamoja na kutoa ushauri wa kisera kwa wadau hao.

Dkt. Abbasi ametoa maagizo hayo leo Novemba 21,2020 Jijini Dodoma katika kikao na Idara hiyo ambapo ameitaka Idara hiyo kusimamia kikamilifu Sekta ya Michezo ambayo inaendelea kuiletea heshima Taifa.

“Ni lazima mkutane na Wadau wenu ili mjue wana mawazo gani katika sekta hii na nyie mtoe ushauri wa kitaalamu ambao utaleta tija katika Sekta hii. Ni lazima muwaeleze Wadau Sera ya Michezo inasemaje kwa sababu nyie ndio mnaoisimamia”, alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameitaka Idara hiyo kuhakikisha kila Shirikisho au Chama kinawasilisha Mpango Mkakati katika Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambao pamoja na mambo mengine, utaonyesha Kalenda ya mwaka katika ligi za kitaifa, kimataifa pamoja na timu ya Taifa lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwepo na uelewa wa pamoja kwa wadau wote utakaoleta mafanikio zaidi katika sekta hiyo.

Dkt. Abbasi amesema kuwa Taifa lazima liwe na ushiriki wa mashindano ya michezo ambao utaleta tija, hivyo Idara hiyo ina jukumu la kuhakikisha mashindano yote ambayo nchi inashiriki katika ngazi mbalimbali yanakua na manufaa, ameongeza kuwa katika mashindano mbalimbali ikiwemo Olympiki lazima kama nchi kujua aina ya michezo ya kushiriki.

Vilevile, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ni mashindano ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa yanazalisha vipaji vingi, hivyo Idara ya Michezo ina jukumu la kusimamia mashindano hayo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo TAMISEMI na Wizara ya Elimu ili vijana wanaofanya vizuri waendelezwe kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya pamoja na sehemu nyingine.

Kwa upande mwingine Katibu Mkuu huyo amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta ya Michezo unaendelea kuimarika ikiwemo kuimarisha Kombe la Mapinduzi.

Cc @wizara_habaritz

,

Comments (0)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *